Monday, October 8, 2012


Na: Onesmo Ngowi

 Masumbiwi au kwa majina mwengine ndondi au ngumi na kwa majina ya mitaani ndogwa, mawe n.k. ni mchezo unapoendwa sana na watu wengi. Aidha mchezo huu ni kati ya michezo inayoogopwa sana duniani. Mchezo wa ngumi uko hatarini kupoteza maana yake ya asili yaani kucheza kama burudani, kuwakilisha nchi na kujenga ushupavu wa mchezaji.

 Mamilioni ya watu wanaojazana kuutazama wasingependa kabisa kujiingiza kuucheza mchezo wa ngumi. Sasa endelea…! Kama nilivyokwisha kusema kuwa kiwango kidogo cha elimu huchangia sana kwenye matatizo haya. Wengi wao hudanganywa fedha zao na mameneja wajanja kwa kusaini mikataba feki. Mameneja hawa husaini mikataba ya kweli wao wenyewe na kutengeneza mikataba mingine ambayo huonyesha kiasi cha kidogo zaidi cha fedha ambayo husaini na mabondia hawa. Kwa mfano promota wa ngumi nje anatuma mkataba unaoonyesha kuwa bondia atayecheza atalipwa dola za Kimarekani elfu kumi (10,000).

 Mkataba huu unapofika menaja huyo hufoji sahihi ya bondia na kuurudisha kwa promota huyo wa nje. Baada ya kuhakikisha kuwa pambano lenyewe limeshapatikana hutengeneza mkataba mwingine wa bondia husika unaoonyesha kuwa malipo ya pambano ni dola za Kimarekani elfu mbili na mia tano au elfu tatu (2000 au 3000). Kwa kuwa wengi wa mabondia hawa hawakubahatika kujua kusoma au kuzungumza lugha ya Kiingereza wanapofika nchi ya mpambano huwa wanapelekeshwa tu na kuwaachia mameneja hawa wakifanya kila kitu. 

Inasikitisha kwamba pamoja na kumwibia zaidi ya dola za Kimarekani elfu saba (7000) katika mkataba huo bado anamkata asilimia 32 mpaka 40 ya fedha alizobaki nazo bondia. Masikini wengi wa mabondia hawa hawajawahi kuvuka mpaka wa Tanzania, hivyo kwao inakuwa ni bahati kuweza kufika nje ya nchi, kupanda ndege, kula vizuri na kulala kwenye hoteli kubwa ambazo kwao ni ndoto ya alinacha kama hawakuwa mabondia.

 Wengi wao huridhika na hali hii na ndiyo maana hawabadiliki na matokeo yake hubakia kuwa fukara hadi uwezo wao wa ngumi unapokwisha. Kama nilivyokwisha eleza hapo mwanzo mojawapo ya kazi za chama cha ngumi za kulipwa hapa nchini ni kutoa leseni na vibali vya mapambano. Hii inajumuisha pamoja na kuhakiki mikataba ya kucheza ngumi. Hivyo kwa kawaida mikataba yote inatakiwa ihakikiwe na chama cha ngumi kabla ya bondia kucheza. Hili ndilo jambo ambalo linachangia sana kwenye migogoro isiyoisha kwenye mchezo wa ngumi za kulipwa.

 Kwa kutambua wazi kwamba mara tu mikataba hii inapohakikiwa na chama itakuwa vigumu kumwibia bondia, wengi wa mameneja hawa wajanga hutumia muda wao mwingi na fedha kuanzisha migogoro dhidi ya uongozi wa chama cha ngumi za kulipwa. Ipo mifano mingi ambapo mameneja hawa wajanja wameenda mbali hata kulipa fedha za kufungua kesi mbalimbali mahakamani kwa lengo la kudhoofisha uongozi wa ngumi za kulipwa ili waendelee kuwatumia mabondia kama mitambo ya kuwazalishia fedha. 

Mabondia nao kwa kutofahamu haki zao ama kwa ajili ya uwezo mdogo wa kuelewa au njaa kali wanakuwa rahisi kuingia kwenye udanganyifu huu. Watu hawa wajanja kwa kutumia fedha wanazopata kutokana na udanganyifu huu kuwabadili mawazo na muelekeo baadhi ya wasimamizi wa vyombo vinaosimamia masuala ya mchezo wa ngumi. Imekuwa rahisi mno kwa wahusika wengi kuyumbishwa kama vile hawajui hali halisi. Hali hii inasababishwa na rushwa inayotolewa na watu hawa wajanja. 

Wengi wa watu hawa hutumia nafasi zao kuwayumbisha mabondia na baadhi ya viongozi wa chama cha ngumi. Hali hii japokuwa kwa sasa imedhibitiwa, kwa kiasi kikubwa imechangia sana kudhoofisha mchezo wa ngumi. HATMA YA TANZANIA KWENYE MEDANI YA KIMATAIFA. Ni wazi kwamba mabadiliko makubwa yanatakiwa yafanyike ili kuunusuru mchezo wa ngumi za kulipwa usiendelee kudumaa. 

Mabadiliko haya yanatakiwa yaanzie kwenye shina lenyewe la ngumi ambalo ni mabondia. Ni lazima kufanyike mabadiliko ya mfumo wa kumpatia bondia mzuri atakayeweza kuvutia wapenzi wengi wa ngumi. Bondia mzuri akishapatikana na kuweza kuvutia watu wengi wanaopenda ngumi ni rahisi kuweza kutengeneza miundo mbinu mingine inayotakiwa kuendeleza ngumi.

 Watu wengi wenye uwezo wa fedha watavutiwa na kuwekeza kwa mabondia hawa na kuwa mameneja wao pamoja na mapromota. Sio rahisi mtu yeyote mwenye akili timamu kuwekeza fedha zake kwa bondia asiyeweza kuzizalisha fedha hizo. Ni vigumu sana kwa mtindo wa sasa wa mabondia wanaokubali kucheza mapambano ya nje kwa lengo la kujipatia tu fedha badala ya ushindani. Mabondia wa aina hii sio rahisi kupata mapambano mengi. Mapambano mengi ya nje ya nchi hususan Marekani, Ulaya, Asia na Afrika ya Kusini hurushwa moja kwa moja na televisheni za nchi zao.

 Mapambano haya hudhaminiwa kwa fedha nyingi hivyo watazamaji na wadhamini wanataka kuona ushindani mzuri. Bondia anapojirusha chini au kukataa kuendelea anadihirisha wazi kwamba hakujiandaa na mpambano wenyewe. Itakuwa vigumu sana kwa bondia kama huyu kupata tena pambano lingine hivyo kuwapa waandaaji wakati mgumu wa kujisafisha. Japokuwa sio kazi za Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa TPBC kuwatafutia mabondia wa Kitanzania mapambano, kwa kuwa mameneja na mechi meka ndio wanaotakiwa kuwatafutia, Kamisheni imejaribu sana kufanya kazi hii kwa ukosefu wa watu hao. Lakini mabondia wengi wa Kitanzania wamejipunguzia nafasi nyingi za kucheza nje baada ya kupoteza mapambano mengi bila ushindani kinyume na mchezo wa ngumi ambao unahitaji ushindani mkubwa. Mabadiliko yametakiwa yaanze kuweka kiwango cha wakati bondia anapotakiwa kujiunga na ngumi za kulipwa. 

Ili kuhakikisha hili, Vyama vya Ngumi za Ridhaa na Kulipwa (BFT na TPBC) vinatakiwa vishirikiane kwa karibu sana kwa kuweka na kusimamia programu endelevu itakayowaandaa mabondia hawa. Ikumbukwe kwamba hapo mwanzo nilieleza jinsi bondia aliyecheza mapambano ya ridhaa kwenye michezo ya Olimpic na Jumuiya ya Madola anavyopata nafasi nzuri kwenye ngumi za kulipwa. Ni muhimu kuwa na mfumo ulio wazi wa kuwaelimisha mabondia kwamba mafanikio yao kwenye ngumi za kulipwa yanategemea msingi wao kwenye ngumi za ridhaa. 

Mfumo huu utawashawishi wadau mbalimbali pamoja na makampuni ya biashara kujiingiza kupromoti ngumi kwa ajili ya mvuto utakaokuwako. Uvuto huu utatokana na ushindani utakaoonyeshwa na mabondia watakaoshiriki kwenye mapambano mbalimbali ndani na nje ya nchi. Aidha mfumo mzuri utajenga msingi mzuri ambapo mabondia wetu watakuwa wanalipwa vizuri kwenye mapambano yatakayochezwa hapa Tanzania.

 Kama nilivyokwishaeleza kuwa nchini Afrika ya Kusini kuna mitandao mikubwa ya televisheni ambayo hurusha pambano moja kwa moja au baada ya pambano la ngumi. Kwa mfumo huu makampuni mengi yatawekeza kwa mabondia wenyewe au kudhamini michezo / mapambano mbalimbali na kuwahakikishia malipo mazuri ya kila pambano. Sio nje ya nchi tu bondia anatakiwa alipwe feha nyingi hata hapa kwetu Tanzania mabondia wetu wataweza kulipwa fedha nyingi kama mfumo huu ukuwepo.

 Kadhalika mfumo mzuri utawaengua wababaishaji waliokwisha kujitokeza kuwatumia mabondia kama vyanzo vyao vya mapato. Wababaishaji hawa ni pamoja na wanaojiita mameneja wa ngumi ambao hata mmoja kufuatana na kumbumbuku za TPBC hawana leseni. Kwa maana nyingine hadi naandika makala haya hakuna Mtanzania yeyote aliye na leseni hai ya kumeneji bondia. Wanaojiita mameneja wanafoji wadhifa huo.

 Mtu huwezi kujiita mfanyabiashara kama huna leseni ya kufanyia biashara hiyo toka TRA. Leseni za ngumi za kulipwa zinatolewa na mamlaka husika. Mfumo mzuri wa ngumi utaiwezesha TPBC kusimamia kwa uhakika na kwa makini taratibu, kanuni na sheria zinazouendesha. Sheria hizi ni pamoja na kuwataka watu wote wanaojihusisha kwenye mchezo wa ngumi za kulipwa kukata leseni ya kufanya hivyo. Nilieleza hapo mwanzo kuwa watu wafuatao wanahusika kwenye mchezo wa ngumi na muhimu wakapata leseni ili watambuliwe na mamlaka husika. 

Watu hawa ni; Mabondia, Mapromota, Mameneja, Makocha, Masekonda, Madaktari, Marefarii, Mechi meka, Timekeeper, Majaji, Ring Announcer, TV Commentator, Waandishi, Boxing Boosters, Mahotel yanayopromoti n.k. Waliotajwa hapo juu wanafaidika kifedha moja kwa moja kutokana na ushiriki wao kwenye mapambano ya ngumi, hivyo hawana budi kupata leseni kutoka kwenye mamlaka husika. Kadhalika. Mfumo huu huu mpya utaleta sura mpya kwenye medani ya ngumi za kulipwa na kuwaweka mabondia ambao kwa kawaida ndio waajiri kwenye nafasi nzuri ya kufaidika na mapato yatokanayo na mapambano wanayoshiriki. 

Vile vile utajenga msingi mzuri wa mabondia wetu kushiriki vyema kwenye medani ya ngumi ya kimataifa na hivyo kuwa washindani badala ya walivyo washiriki tu kwa sasa. Vile vile katika mfumo huu mpya semina mbalimbali za kuwaelimisha wadau wa ngumi zitafanyika na hivyo kutoa nafasi kwa watanzania wengi kushiriki kwenye mchezo huu. Vyama vya ngumi za ridhaa na kulipwa vikishirikiana kwa karibu vitasimamia vyema mabondia walio kuwa tayari kuhama kutoka kwenye ngumi za ridhaa na kujiunga na ngumi za kulipwa kwa faida ya nchi. 

Itaendelea…! Mwandishi wa makala haya ni; Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Shirkisho la Ngumi za Kulipwa Afrika Mashariki na Kati (ECAPBF)

0 comments:

Post a Comment