Monday, October 15, 2012Mshindi wa Top Model Redd's Miss Tanzania 2012,Magdalena Roy (katikati anaepungia mkono) akiwa na washiriki wenzake alioingia nao hatua ya tano bora katika shindano lililomalizika usiku wa kuamkia leo kwenye ukumbi wa hoteli ya Naura Springs,Jijini Arusha.
MISS Dar City Center ambaye pia alishika nafasi ya pili katika shindano la Redd’s Miss ilala, Magdalena Roy amefanikiwa kuingia 15 Bora ya Redd’s Miss Tanzania baada ya juzi usiku kufanikiwa kutwaa taji la Top Model.
 
Magdalena anakuwa mshindi wa pili kuingia katika hatua hiyo, akiungana na Miss Mbulu, Lucye Stephano ambaye wiki iliyopita alitwaa taji la Miss Photogenic.
 
Katika shindano la Top Model lililofanyika kwenye hoteli ya Naura Spring, mjini hapa lilikuwa na upinzani mkali kutoka kwa washiriki wote wa Redd’s Miss Tanzania.
 
Mbali na Magdalena warembo wengine waliofanikiwa kuingia katika tano bora walikuwa ni Mary Chizi (Ilala), Irene Veda (Lindi), Belinda Mbogo (Dodoma) na Sina Revocatus (Elimu ya Juu).
 
Akizungumza na gazeti hili mjini hapa jana, Afisa Habari wa Kamati ya Miss Tanzania, Haidan Ricco alisema warembo hao jana waliondoka kuelekea Tanga kwa ajili ya kutembelea mapango ya Amboni, kabla ya kurejea Dar es Salaam.
 
Warembo wapatao 30 wanawania taji la Redd’s Miss Tanzania, ambalo kwa sasa linadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Redd’s Original.

0 comments:

Post a Comment