Monday, October 8, 2012
 Na Elizabeth John
MKURUGENZI wa Misitu na Nyuki, chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Felician Kilahama (Pichani kushoto),  amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Shughuli za Misitu Duniani ambapo ataiwakilisha Afrika kwa kutumia bendera ya Tanzania, chini ya mfuko wa chakula na kilimo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kilahama alisema katika kikao cha 21 kilichohudhuriwa na Kamati ya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), kilichofanyika nchini Italia wiki iliyopita, kulingana na kanuni za utaratibu wa kamati, ikaamua kumchagua Mwenyekiti kutoka miongoni mwa wanachama wake.
Kilahama alisema anajisikia furaha sana kuchaguliwa katika idara hiyo na kwamba Watanzania wanapaswa kutambua kuwa, hawakufanya makosa kumchagua yeye, kwani ana uhakika bendera ya Tanzania itapepea vema.
“Watanzania inatakiwa mniombee kazi hii sio ndogo, kikubwa ambacho tutakuwa tukikifanya ni kuleta maendeleo ya misitu, pamoja na kujua tutapunguzaje gharama za matumizi ya nishati, kama kuni na mkaa bila kukata miti na kupunguza misitu kitu ambacho kina athiri mazingira,” alisema Kilahama.
Alisema, kwa kawaida anayetaka uongozi katika shirika hilo huwa anatuma barua ya maombi kwa uongozi husika kwa kushirikiana na uongozi wa nchi yake, jina lake likipitishwa ndio atachaguliwa na wanakamati wa shirika hilo.
“Kiukweli ilikuwa kama miujiza, aliyekuwa amechaguliwa alikuwa ni Mnigeria alishindwa kutokana na sababu ambazo zipo nje ya uwezo wake na Mnamibia alikosa viza ya kuingilia nchini Italia, hapo ndio nikachaguliwa mimi kwa asilimia zaidi ya 120,” alisema.
Aliongeza kuwa, kazi hiyo ataifanya kwa muda wa miaka miwili na amewataka Watanzania wamuombee katika shughuli hizo ambapo anaimani itakuwa ni faida ya nchi nzima kwa ujumla.

0 comments:

Post a Comment