Saturday, October 13, 2012
USHINDI kutoka kwa Toto African ya Mwanza katika mechi ya juzi kwenye Uwanja wa CCM- Kirumba, umewapa usongo mabingwa hao mara 24 wa Bara tangu mwaka 1965, ambapo sasa wameapa hakuna kulala katika vita ya ubingwa wa Ligi Kuu.
Ikitoka kulimwa bao 1-0 na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, juzi ilizinduka na kushinda mabao 3-1, hivyo kufikisha pointi 11, ikiwa nafasi ya tatu nyuma ya kinara Simba na Azam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrance Mwalusako alisema kikosi cha timu hiyo kilitarajiwa kuwasili jana usiku, kuendelea na mazoezi yake ya kujiandaa na mechi yake dhidi ya Ruvu Shooting itakayocheza Oktoba 20.
Mwalusako, beki wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, alisema Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ernie Brandts, ataanza rasmi progamu yake kwani kikosi chake kitakuwa kamili, hivyo kubaini dosari zilizojitokeza kwenye mechi kadhaa zilizopita.
“Unajua tangu kocha aanze kazi, hajapata muda wa kutosha kuwajua vizuri wachezaji, hivyo kwa siku za kujiandaa na mechi ya Ruvu Shooting, ataangalia maeneo gani yatapaswa kufanyiwa kazi ili kupata matokeo mazuri kwenye mechi zijazo,” alisema.
Mwalusako aliongeza kuwa, ushindi kutoka kwa Toto ni faraja, na kitu muhimu kwao ni kuongeza juhudi zaidi kushinda mechi zijazo kuzidi kujiongezea pointi.
Katika hatua nyingine, Mwalusakao alisema wameandika barua kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuomba mechi yao kuhamishwa kutoka Azam Complex hadi Uwanja wa Taifa kwa hoja ya kutoa nafasi kwa wapenzi na mashabiki wengi kushuhudia.

0 comments:

Post a Comment