Wednesday, January 15, 2014


IMG_9189 
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na vijana katika moja ya matukio.
………………………………………………………
Na Benjamin Sawe WHVUM
 “Vijana ni nguvu kazi ya Taifa”. Hii ni kweli na kwa mujibu wa
utafiti wa Nguvu Kazi Nchini ya mwaka 2006 asilimia 68% ya nguvu kazi nchini ni Vijana ambao idadi yao kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ni 15,587,621 sawa na asilimia 34.7% ya idadi ya watu wote nchini. Kati yao Vijana wa kike ni 8,273,505 sawa na asilimia 35.9% na Vijana wa kiume ni 7,314,116 sawa na asilimia 33.4%.
Kutokana na umuhimu huu, kumekuwa na jitihada mbalimbali za Serikali zinazolenga katika masuala ya maendeleo ya Vijana nchini hii ikiwa ni pamoja na kuwa na Sera, Mipango na Mikakati inayokidhi mahitaji mbalimbali ya vijana kama vile, Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana 2007,Sera ya Taifa ya Ajira 2008 (Iliyo chini ya Wizara ya Kazi na Ajira), Mpango Kazi wa Taifa wa Ajira kwa Vijana 2007 na Programu ya Kukuza Ajira zenye Staha kwa Vijana nchini inayoratibiwa kati ya Wizara Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Bw. James Kajugusi anasema Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana 2007 ni matokeo ya maboresho ya Sera ya Vijana ya mwaka 1996 ambapo, maboresho ya Sera hiyo yanatokana na mabadiliko, mahitaji au changamoto mbalimbali zinazojitokeza za kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Vilevile, suala la ukuaji wa kasi ya Sayansi na Teknolojia huilazimu Serikali kufanya maboresho muhimu ili kuendana na wakati. Anasema Bwana Kajugusi. Anafafanua kuwa msukumo mwingine unaopelekea kufanyika kwa maboresho ya Sera ni pamoja na utekelezaji wa maazimio yanayofikiwa na Tanzania ikiwemo kama vile Jumuiya ya Madola, Umoja wa Mataifa, EAC, SADC na AU.
Aidha kwa upande mwingine Sera hutoa Mwongozo na Dira kwa wadau mbalimbali kuweza kutekeleza yale ambayo yametamkwa kwenye Sera hiyo. Hivyo, Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana 2007 inatoa fursa kwa vijana kujiamini na kujitambua.
Bwana Kajugusi anasema, Ibara ya 3(3), Sera inatamka kuwa “kutakuwa na utaratibu wa kutoa mwongozo kwa ajili ya kuwezesha malezi sahihi ya Vijana na kuendeleza vipaji vya Vijana”.
Hivyo katika kutekeleza tamko hilo la Sera, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya Vijana nchini imeweza kuandaa programu za kuwawezesha Vijana kujiamini na kujitambua kama vile “Programu ya Stadi za Maisha kwa Vijana Nje ya Shule”
Anasema Vijana wengi waliopata elimu hiyo, wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kubadili fikra na kuchukua hatua ya maendeleo katika kufanyia kazi vipaji walivyokuwa navyo ambapo ni sehemu mojawapo ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana 2007. Pia Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana 2007 vilevile inatambua umuhimu wa ushiriki na ushirikishwaji wa Vijana katika kubaini na kutumia rasilimali zilizopo kwa ajili ya ustawi wa maendeleo yao na ya nchi kwa ujumla.

0 comments:

Post a Comment