Wednesday, October 29, 2014


Francis Boniface Cheka 'Maputo'
Na Imani Makongoro, Mwananchi
Nyumbani kwa bondia Francis ‘SMG’ Cheka hakuishi pilika ambazo zinatokana na kazi ya chupa za plastiki anayofanya bingwa huyo wa zamani wa dunia wa WBF.
Nje ya nyumba yake kuna mafurushi kila kona yakiwa na ‘bidhaa’ tofauti ikiwamo chupa za plastiki, chupa za konyagi, chibuku na plastiki ngumu (ndoo na madumu) yaliyopasuka.
Cheka anavyookota chupa
“Mimi ndiyo mwanzilishi wa biashara hii hapa Morogoro, niliianza 2004 baada ya kuamua kuingia mtaani kuokota na kuziuza mwenyewe, wakati huo kilo moja niliuza kwa Sh100 na nilikuwa nikizunguka kutwa nzima kutafuta chupa mtaani,” anasema Cheka.
Anasema wakati anaanza kuokota chupa alikuwa na miaka mitano tangu aingie kwenye ngumi za kulipwa, lakini hakuwa maarufu.
“Nilikuwa nina uwezo wa kuzunguka na kuokota hadi kilo 100 kwa siku, japo ilikuwa kazi ngumu, lakini nilipata fedha nikanunua kiwanja maeneo ya Kilimahewa na kujenga nyumba kwa kazi ya kuokota chupa.
“Pia niliweza kujiandalia mapambano peke yangu kwa kazi hii, ambayo yalinijenga na kunipa umaarufu kwenye ngumi, nimejiandalia mapambano zaidi ya 15 kwa fedha niliyopata kwa kuokota chupa,” anasema Cheka.
Anasema vijana wengi wa Morogoro walianza kuokota chupa baada ya kuona Cheka amejenga nyumba kwa kazi hiyo, hivyo hakuwa na hiyana aliwafundisha kazi hiyo na wengine aliingia nao mtaani kuokota.
“Nilipoanza kucheza mapambano ya ubingwa wa Afrika nilisimama kuokota chupa nikawaachia wengine na mimi kuelekeza nguvu zangu kwenye ngumi, kijiwe changu nikamweka mtu wa kufanya hiyo kazi na nikawa na nanunua kwa watu wengine kisha mimi nauza tena.
“Kwa kipindi chote ambacho nilikuwa nimebanwa na masuala ya ngumi, mradi wangu huu uliyumba kwani kila niliyemwachia alikuwa na fikra za kuniibia, ilifikia mahali nikakwama kwani nilikopa fedha benki kuongezea nguvu kwenye biashara yangu ya makopo hivyo nilipaswa kulipa,” anasema Cheka.
Anavyookota chupa mtaani
“Watu wanashangaa mtu kama mimi kuokota chupa, lakini ndiyo kazi inayoniweka mjini, wiki iliyopita nilikuwa Msamvu (stendi kuu ya Morogoro) nakusanya chupa kwa bahati nikakutana na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia alishangaa kuniona naokota Chupa.
“Hakuamini kama mimi bingwa wa dunia na bondia namba moja Tanzania ndiyo naokota chupa mtaani, lakini ukweli nisipofanya kazi hii na nikabaki kutegemea ngumi, maisha yatakuwa magumu kwangu,” anasema Cheka.
Anasema haoni aibu kufanya kazi hiyo kwani ni kazi iliyompa mafanikio na kujenga nyumba mbili, moja ikiwa Kilimahewa ambako anaishi hivi sasa na nyingine Kihonda alikowapangisha watu wengine.
“Muda wangu mwingi nimeelekeza kwenye chupa, mazoezi sasa sifanyi kwani nina muda sijafanya mazoezi ya ngumi, nasimamia mwenyewe biashara yangu ya chupa ambayo mbali na kuokota mwenyewe pia kuna watu ambao wanaokota na kuniuzia.
“Chupa za maji nanunua kilo moja Sh250 na mimi nauza 700 baada ya kusaga, kwa mwezi nina uhakika wa kuuza kilo 4,500 mpaka 6,000 na plastiki ngumu nanunua Sh350 na mimi nauza Sh 2,000 baada ya kusaga hivyo kwa mwezi nauza zaidi ya kilo 3,000, pia naokota chupa za konyagi na chibuku ambazo naziosha na kuwauzia watu wa kampuni hizo,” anasema Cheka.
Ameamua kuingia mtaani kutembeza CD
“Sijapata mafanikio yoyote kwenye ngumi hadi sasa hivyo nimeona nijaribu kuuza CD za mapambano yangu labda nitafanikiwa,” anasema Cheka.
Anasema kazi hiyo anaifanya kwa kutembeza CD zake mkononi na kuwapelekea watu kwenye maeneo tofauti mjini Morogoro na amekwishauza CD 200 hadi sasa.
“Nilitoa CD 200 ambazo niliziuza kwa kutembeza mwenyewe mkononi zikaisha na sasa nimetoa nyingine 200, najitangazia biashara mwenyewe kwani napeleka kwenye mkusanyiko wa watu, vituo vya daladala, Stendi ya Msamvu na maeneo ambayo najua nikienda sikosi wateja, CD moja nauza Sh 3000,” anasema Cheka.
Fedha nyingi aliyowahi kupata katika ngumi
“Fedha nyingi niliyopata ni Sh10 milioni ambayo nilicheza pambano Russia mwezi Desemba 2012 na kupigwa kwa Knock Out (KO) raundi ya nne, pambano lile nilicheza bila kujiandaa na nilipata fedha hiyo kwa kuwa sikuitumia kwenye maandalizi,” anasema Cheka.
Anasema mapambano mengi anayocheza nchini amekuwa akiambulia Sh3 milioni mpaka Sh4 milioni baada ya kutoa fedha za maandalizi, kumlipa kocha na kununua vifaa.
“Pambano nililocheza na Mmarekani la ubingwa wa dunia nilipewa Sh4 milioni za maandalizi, nikaweka kambi Nairobi kila kitu nalipa mwenyewe mpaka kumlipa kocha, hadi narudi sina fedha baada ya pambano nikapewa Sh3 milioni, nilikuwa na madeni nikalipa na kubaki sina kitu.
“Hata wakati nafanyiwa sherehe ya kupongezwa Morogoro, sikuwa na hata shilingi, siku nawekewa dau la Sh10 milioni nikacheze Russia, sikukataa japo nilijua sina mazoezi, nilipigwa KO kihalali na kuvuliwa ubingwa wa dunia,” anasema Cheka.
Mkakati wake wa kurudi shule
Cheka alipewa ofa ya masomo kwenye Chuo cha St Joseph cha mjini Morogoro na aliingia darasani siku moja kisha akatokomea hadi leo hajawahi kurudi.
“Mimi ni baba wa familia ambayo inanitegemea, siyo kama sipendi kusoma, lakini nikiwa shule majukumu ya familia nitayatekeleza vipi? Hivi sasa nimeamua habari ya kusoma niiweke kando niboreshe biashara yangu, Mungu akiniweka hai, nitasoma miaka ijayo,” anasema Cheka.
Kwa nini anaitwa Kazimoyo?
Akiwa Morogoro, Cheka anajulikana pia kwa jina la Kazimoyo.
“Hili jina nimepewa na marafiki zangu ambao wananiita Kazimoyo kutokana na kazi ninazozifanya, ambazo wanasema nina moyo mgumu ndiyo sababu nazifanya, hivyo kazi ninazofanya sasa na nilizowahi kufanya nimefanya kwa moyo tu,” anasema Cheka.
Historia fupi ya maisha yake
Cheka alizaliwa miaka 32 iliyopita jijini Dar es Salaam, akiwa mtoto wa kwanza kwa baba yake, Boniface Cheka na alisoma Shule ya Msingi Kinondoni Hananasifu.
Alianza kucheza ngumi akiwa darasa la tatu na wakati huo baba yake alipenda kumfundisha ngumi.
“Nilipohitimu shule ya msingi, nilipata kazi kwenye gari la taka la Manispaa ya Kinondoni, nilifanya kazi hiyo pia nikijifua ngumi kwenye Ukumbi wa Arnautoglu, Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
“Baada ya kuona maisha magumu Dar es Salaam, Nilikwenda Morogoro, sikuwa na mahali pa kufikia hivyo nikaomba kazi ya kufagia Stendi ya Msamvu na usiku hapo ndipo nikawa nalala,” anasema Cheka.
Anasema alilazimika kutandika maboksi na kulala kituoni hapo usiku ulipoingia na asubuhi anaamkia kwenye kibarua cha kufagia kituo hicho.
“Nilipata fedha kidogo na kupanga chumba, nakumbuka kitanda changu nilinunua kwa fedha niliyopata kwenye kazi ya kuzibua choo, sikuwa na ujuzi huo, lakini rafiki zangu waliponiambia kuna kazi hiyo nilienda kufanya na kulipwa Sh50,000 ambayo ilikuwa fedha nyingi kuwahi kulipwa,” anasema Cheka.
Anasema baada ya muda ndipo aliingia mtaani kuokota chupa, kazi iliyompa mafanikio na kujenga nyumba, na kutumia fedha aliyopata kujitangaza kwenye ngumi.
CREDIT: MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment