Sunday, January 17, 2016


KIKUNDI cha Wanaume wapiga makasia cha Costantine Lusalago cha Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza,kimetwaa ubingwa wa mashindano ya  mbio za mitumbwi za Balimi Boat race 2016 na kujinyakulia kombe, medali za dhahabu na kitita cha sh.1,200,000.

Pia, kikundi cha Tabu Daud kutoka Wilaya ya  Misungwi,kiliibuka kidedea na kukabidhiwa kombe,medali na feda taslimu sh 1,000,000 baada ya kushika nafasi ya kwanza kati ya  11,kwenye mashindano hayo  yanayodhaminiwa na kampuni ya Bia nchini (TBL) kupitia bia ya Balimi Extra Lager.
Katika mashindano hayo ya kupiga makasi yaliyofanyika  kwenye ufukwe wa Annex Riverside Igombe, kikundi cha nahodha Daniel Peter ,kutoka Misungwi kilishika nafasi ya pili kwa wanaume,nyuma ya mabingwa hao wa mwaka 2015  na kuzawadiwa sh.1,000,000.
Nafasi ya tatu ilinyakuliwa kikundi cha nahodha  Dotto Kisariba kutoka Kigoto Ilemela, na kukabidhiwa sh.800,000 na nafasi ya nne,ilikwenda kwa mtumbwi wa nahodha Musa Misalaba kutoka Sengerema na kuondoka na sh.600,000.
Vikundi vilivyoshika nafasi ya tano hadi ya kumi ambavyo ni vya Elisha, Muinja Nyabalala,Joseph Jacob,Jah Benard,Kinde Paulo na Sijaona, vilipata kifuta jasho cha sh.250,000 kila kimoja.
Nafasi ya pili kwa wanawake ilikwenda kwa kikundi cha Frola Bahati na kuapata sh.800.000,nafasi ya tatu ilichukuliwa na kikundi cha Bertha Aloys cha Misungwi na kuzawadiwa sh.600,000 na nafasi ya nne ilinyakuliwa Mispina Hussein ambacho kilipewa sh.400,000.
Hata hivyo katika mashindano hayo kikundi cha nahodha Yasinta kutoka Kirumba mtumbwi wazo ulipinduka na kuzama lakini baada ya kuokolewa walibadili mtumbwi na kuendelea mashindano na ukashika nafasi ya tisa.
Washindi wa nafasi ya tano wanawake ambao ni Angelina John,Bhoke Salala,  Lucy,Yasinta,Salome na Rehema walipata kifuta jasho cha sh.200,00o kila kikundi.
Afisa Utamaduni na Michezo wa Manispaa ya Ilemela Kizito Bahati ,ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya, hiyo, Manje Msambya,aliushukuru uongozi wa TBL na kuutaka usifanye mashindano hayo kuwa tukio la mara moja kwa mwaka.
Pia alivitaka vyama vya mchezo huo kuhakikisha vinaendesha ligi za wilaya ,wakishirikisha vikundi/vilabu vya wachezaji wenye taaluma kama ilivyo kwenye mchezo wa soka na mingine,ili timu imara zipatikane zitajkazoweza kushindana kimataifa hasa ukanda wa Afrika Mashariki.
Naye Maneja Mauzo wa TBL Kanda ya Ziwa, Godwin Zacharia,alisema kuwa, kampuni hiyo inalenga kuwa karibu na jamii ya wavuvi ili kuendeleza rasilimali ya uvuvi na kuifanya iendelee kuwepo kwa manufaa na maslahi ya jamii na vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa upande wake Meneja wa Fedha TBL Kanda ya Ziwa, Nancy Riwa,aliwapongeza wanawake walioshiriki mashindano ya mwaka huu,kwa kuonyesha kuwa wana uwezo na nguvu ya kupiga makasia.
Aidha, Mwenyekiti wa Chama cha Mitumbwi Taifa, (Tanzania Canoe Assocition) ,Richard Mgabo,alisema TBL ina stahili pongezi hivyo iendelee kuyapa heshima mashindano hayo ya mbio za Mitumbwi  za Balimi,ili yakidhi mahitaji ya wadau wa mchezo huo.
 Mashindano hayo yamefikisha umri wa miaka 15 tangu yaanzishwe mwaka 2001chini ya udhamini wa TBL kupitia kinywaji chake cha Balimi Extra Lager,ambapo mwaka huu yameboreshwa kwa kufanyika kwa hadhi ya kimkoa kwa mikoa wa kanda ya ziwa, huku wilaya ya Ukerewe ikipewa hadhi ya kuwa mkoa kwenye michuano hiyo ya kupiga makasia.

0 comments:

Post a Comment