Friday, July 29, 2016SALAAM ZA RAMBIRAMBI MSIBA WA JOSEPH SENGA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepokea kwa masikitiko na mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha mmoja wa waandishi wa habari za picha mwandamizi na mahiri nchini, Joseph Senga kilichotokea usiku wa jana akiwa kwenye matibabu nchini India.

Kama taasisi na kisha mtu mmoja mmoja kuanzia kwa wanachama na viongozi wa chama kwa hatua ya sasa tumejikuta tumeishiwa maneno ya kusema kuhusu kifo cha mwandishi huyu mwandamizi, lakini katikati ya mshtuko na majonzi tuliyonayo, tunaweza kusema kuwa kifo cha Senga, hasa siku kiliyotokea, kimedhihirisha jambo moja kubwa kuwa alikuwa SHUJAA WA DEMOKRASIA NA HAKI.

Kifo cha Senga kimetokea siku ambayo kulikuwa na matukio makubwa mawili kuhusu demokrasia na haki nchini.

Kwanza, wakati Senga anafariki usiku wa Jumatano, Julai 27, mchana wa siku hiyo hiyo Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, ilikuwa imetoa hukumu ya kifungo cha miaka 15 jela askari anayefahamika kwa jina la Pacificius Simon kwa hatia ya kosa la kumuua bila kukusudia aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Channel ten, mkoani Iringa.

Matukio hayo matatu; kuuwawa kwa Mwangosi, hukumu ya aliyemuua na kifo cha Senga, yana uhusiano mkubwa wa karibu huku Senga akiwa katikati yake, kwamba;

Picha zote ambazo hadi leo zinaweza kupatikana dunia nzima kupitia mtandao wa intaneti zikionesha mauaji ya kikatili aliyofanyiwa Mwangosi, kuanzia ile ambayo inaonesha kundi la askari polisi likiwa limemzunguka Mwangosi huku mmoja wao akiwa amemlenga kwa bunduki ya kulipulia mabomu ya machozi, hadi zile ambazo zinaonesha mwili wa mwandishi Mwangosi ukiwa umefumuliwa na kutawanywa vibaya baada ya kulipuliwa, huku nyingine ikimuonesha mmoja wa askari akiugulia maumivu ya ‘bomu’ lililomuua Mwangosi, zilipigwa na Shujaa Senga.

Kwa watu waliokuwepo siku ya tukio hilo baya kuwahi kuikumba tasnia ya habari nchini, watakumbuka kuwa Senga alipiga picha zile akiwa katikati ya mirindimo na moshi wa mabomu, ngurumo za risasi za moto na kundi la askari wengi ambao walikuwa wanazidi hata idadi ya wanachama na viongozi wa CHADEMA waliokuwa wamekusanyika kwa amani kwenye ofisi yao kijijini Nyololo kabla hawajavurugwa na Jeshi la Polisi likiongozwa na RPC Michael Kamhanda.

Picha zile ambazo ziliiambia dunia nzima ukweli wa tukio hilo, ziliokoa watu wengi na bila shaka zilisaidia kutotokea kwa jambo kubwa ambalo watawala walishaanza kuonesha nia ya kulitekeleza, kupitia maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi, makao makuu na mkoani Iringa, ambao walitaka kuonesha kuwa CHADEMA ‘walijilipua’, ambapo maana yake ni kwamba wafuasi, wanachama na viongozi wa CHADEMA walikuwa na milipuko au vitu vya namna hiyo.  

Pili; Senga amefariki siku ambayo Watanzania bila kujali tofauti zao, wakiongozwa na CHADEMA walitangaza Operesheni UKUTA ambayo moja ya malengo yake ni kupigania haki za makundi mbalimbali ya Watanzania, wakiwemo waandishi wa habari dhidi ya mifumo kandamizi inayolelewa na watawala kupandikiza mbegu za utawala wa kidikteta nchini.

Kwa muda mrefu, kupitia chombo chake alichokuwa akikifanyia kazi hadi mauti yanamkuta, Free Media, CHADEMA kama inavyofanya kazi na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali, ilikuwa ikishirikiana na Senga kikazi, huku naye akifanya kazi yake kwa uwezo mkuwa, akizingatia miiko na misingi ya taaluma ya uandishi wa habari, kwa weledi mkubwa. 

Habari picha zake mbalimbali ambazo zimekuwa zikidhihirisha ukongwe wake katika tasnia ya habari, zikiwemo za matukio ya CHADEMA, zitakuwa historia itakayotunza jina lake miongoni mwa waandishi mahiri nchini ambazo waandishi chipukizi watajifunza.

Kwa masikitiko makubwa, CHADEMA inatoa salaam za pole kwa familia ya marehemu, Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Free Media, wafanyakazi wenzake, tasnia ya habari nchini na Watanzania wengi walioguswa na msiba huo. Mwenyezi Mungu awatie moyo wa ujasiri kuyakabili majonzi mazito ya kifo cha mpendwa Senga.

Huyo ndiyo Joseph Senga. Shujaa wa demokrasia na haki. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema.


Imetolewa leo Alhamis, Julai 28, 2016 na;

Tumaini Makene
Mkuu Idara ya Habari na Mawasiliano

CHADEMA

0 comments:

Post a Comment